7 Mei 2025 - 21:36
Source: Parstoday
Imam Khamenei: Ustaarabu wa Kiislamu ni kinyume cha ustaarabu wa sasa wa kimaada

Katika ujumbe wake kwa kongamano la "Miaka 100 wa Kuanzishwa Hauza ya Qum nchini Iran," Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: "Kazi muhimu zaidi ya Hauza na taasisi ya kielimu ya vyuo vikuu vya kidini, ni kufikisha ujumbe wa wazi na kuweka msingi wa ustaarabu mpya wa Kiislamu."

Katika ujumbe huo uliotumwa kwenye kongamano la "Kumbukumbua ya miaka 100 ya kuanzishwa Hauza ya Qum nchini Iran," Imam Ali Khamenei, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amebainisha historia ya kuundwa Hauza hiyo kati ya matukio makubwa na ya kutisha ya mwanzoni mwa karne ya 14 Hijria, na nafasi ya Ayatullah Abdul Karim Hairi katika kuanzisha, kubakisha na kustawisha taasisi hiyo.

Ameongeza kuwa: Mojawapo ya fahari za Hauza ya Qum ni kwamba watu wakubwa kama Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu amrehemu) wametokea katika taasisi hiyo ya elimu, na katika muda usiozidi miongo sita, Hauza hii ilizidisha nguvu zake za kiroho na uungaji mkono wa watu kiasi kwamba iliweza kuutokomeza utawala wa kihaini, fisadi na usio na maadili kwa mikono ya wananachi; Na kurejesha Uislamu katika nafasi yake ya mamlaka ya kisiasa nchini baada ya karne nyingi.

Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa, Hauza si taasisi ya kufundisha na kusoma tu, bali ni mkusanyo wa maarifa, elimu na kazi za kijamii na kisiasa.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa moja ya majukumu muhimu ya Hauza, kama kituo chenye thamani cha kielimu chenye msingi wa kisayansi ya miaka elfu moja, ni kujibu masiala yanayohusiana na utawala wa Kiislamu na namna ya kuongoza jamii. Ameongeza kuwa: Masuala kama vile uhusiano wa dola na watu na dola na mataifa mengine, suala la kupinga udhibiti wa makafiri juu ya Waislamu, mfumo wa kiuchumi na misingi mikuu ya mfumo wa Kiislamu, asili ya utawala kwa mtazamo wa Uislamu, nafasi ya watu ndani yake na kuchukua msimamo juu ya masuala muhimu na dhidi ya mfumo wa kibeberu, dhana na maudhui ya uadilifu na makumi ya masuala mengine ni miongoni mwa mambo yanayopaswa kupatiwa majibu katika Hauza na taasisi ya kielimu ya vyuo vikuu vya kidini. 

Vilevile ametilia mkazo udharura wa Hauza kuwa na ujuzi wa elimu ya dunia ya sasa na kushirikiana na vyuo vikuu, katika kubuni na kudhibiti mifumo ya kijamii.

Imam Khamenei pia ametoa wito kwa wanazuoni wa kidini kushiriki kikamilifu katika kukuza mafundisho ya itikadi za Kiislamu, akiangazia uongozi wa kihistoria wa wanazuoni wa kidini nchini Iran na harakati kubwa za mageuzi za Iraq katika kipindi cha miaka 150 iliyopita.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameutaja ustaarabu wa Kiislamu kuwa ni kinyume cha ustaarabu wa sasa wa kimaada na potofu na akasisitiza kuwa: Kwa mujibu wa kanuni za maumbile, ustaarabu huu batili utatoweka, na wajibu wetu ni kusaidia kusambaratisha batili hiyo na kuandaa ustaarabu mbadala kifikra na kimatendo.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha